Mtoto Wa Mchuuzi Aliyejijengea Ujasiri Kwa Kurasa...
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Kijiji cha Msaranga kilijulikana kwa soko lake dogo lenye kelele nyingi na vumbi la kila asubuhi.
Hapo ndipo alipokulia Amani, kijana mdogo, mtoto wa mchuuzi wa viazi.
Maisha yalikuwa magumu.
Kila siku ilianza kwa sauti ya mama yake akimwamsha mapema:
“Amani, chukua ndoo, twende sokoni.”
Amani alikuwa mpole, mwenye aibu na asiyejiamini.
Kila alipokuwa karibu na watu wengi, sauti yake ilikuwa ndogo kama ya kupiga dua moyoni.
Alipoitwa darasani ajibu swali, alitetemeka. Watu walimcheka. Alijiona dhaifu. Akijisemea moyoni,
"Mimi siwezi kuwa kama wale watoto wanaoongea mbele za watu. Mimi si kitu."
Siku moja, akiwa anafagia meza sokoni, aliona karatasi la gazeti limefungiwa samaki.
Katika lile karatasi, kulikuwa na maneno yaliomvutia:
“Vitabu vinawafanya watu kuwa huru.”
Alishangaa. Akajiuliza, “Inawezekanaje kurasa tu zabadili maisha ya mtu?”
Hapo ndipo moyo wake mdogo ukapata hamu ya kujua zaidi.
Lakini mara akajikumbusha:
“Mimi ni mtoto wa sokoni, siwezi hata kununua kitabu. Hizo ni ndoto za watu wa mjini.”
Alijaribu kusahau. Lakini usiku hakulala. Maneno yale yalimtesa kichwani. Vitabu… vinawafanya watu kuwa huru?
Asubuhi moja, wakati wa mvua, walikimbilia kujikinga kwenye kibanda cha duka.
Ndipo alipokutana na mzee mmoja mwenye duka la vitabu vilivyotumika.
“Unapenda kusoma?” mzee alimuuliza.
Amani akasita, akasema:
“Napenda… lakini sina pesa.”
Mzee alitabasamu:
“Chukua hiki. Ni bure. Ukimaliza, rudi na uniambie ulichojifunza.”
Kilikuwa ni kitabu cha "Think and Grow Rich."
Kwa mara ya kwanza, Amani alisoma ukurasa mzima bila kuogopa.
Kadri alivyosoma, alihisi kama kuna mtu anazungumza naye moja kwa moja.
Alijifunza kuhusu nguvu ya fikra. Akaanza kujiuliza maswali ambayo hakuwahi kujiuliza.
Akaandika ndoto zake kwenye daftari.
Kuna Kitu kilianza kubadilika ndani yake.
Alipoanza kusoma kila siku, baadhi ya marafiki walimcheka:
“Umeanza kuwa msomi sasa?”
“Vitabu haviwezi kufuta umaskini!”
Lakini wengine walivutiwa. Walianza kuja kumuuliza maswali.
Alianza kuwashauri. Polepole, watu walianza kumtambua kama kijana mwenye busara.
Alianza kujiamini. Sauti yake sasa ilikuwa thabiti.
Miaka mitatu baadaye, Amani alialikwa kutoa hotuba ya vijana katika kongamano la wilaya.
Ilikuwa ni fursa ya pekee. Lakini alitetemeka tena. Hofu ya kale ikamrudia.
“Je, nitashindwa mbele ya watu?”
Lakini alifungua kitabu chake cha kumbukumbu, alichokuwa akiandika kila alichojifunza.
Akaona sentensi aliyoiandika zamani:
“Usiogope kushindwa, ogopa kutosimama.”
Siku ya hotuba ilifika. Ukumbi ulifurika.
Alipokamata kipaza sauti, palikuwa kimya kama kaburi.
Dakika ya kwanza ilimpiga kama radi.
Lakini alikumbuka kila alichojifunza.
Akazungumza kwa ujasiri. Alisimulia safari yake ya kijijini, samaki na gazeti, na kitabu cha kwanza.
Ukumbi ukatulia. Watu wakalia. Na walishangilia kwa makofi ya nguvu.
Siku hiyo alipokea barua ya ufadhili wa kusoma chuo.
Lakini zaidi ya yote, alipata zawadi ya kujiamini.
Hakujiona tena kama mtoto wa sokoni. Alijua sasa ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kwa sababu alikuwa na maarifa.
Alirudi kijijini kwake akiwa amevaa suti, siyo kwa majivuno, bali kwa ushuhuda.
Alifungua maktaba ndogo. Aligawa vitabu kwa vijana.
Aliwaambia:
“Hamna aliyezaliwa jasiri lakini kila mmoja anaweza kujijenga kwa kurasa."
Leo hii, Amani ni mshauri wa vijana. Anaandika, anafundisha, na anahamasisha.
Anaona maisha tofauti si kwa sababu alizaliwa na bahati, bali kwa sababu alikubali kujifunza.
Safari yake ni zawadi kwa wengine. Anaamini:
“Kitabu kimoja kinaweza kubadilisha maisha.
Kusoma ni mbegu ya kujiamini.
Na maarifa ni taa ya kufanya maamuzi sahihi.”
Je, na wewe unahisi unakosa kujiamini?
Je, unapata shida kufanya maamuzi?
Kama jibu ni ndiyo, basi tambua…
Safari yako inaweza kuanza kwa ukurasa mmoja tu.
Karibu Kwa Kupiga Au Kutuma Meseji Kwenda 0750376891.
Rafiki Yako Anayekupenda Na Kukujali Sana,
Ramadhani Amir,
Mwandishi|Mkufunzi|Kocha
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni
Chapisha Maoni